WASIA WANGU: WEWE NI BINGWA! JIAMINI

Ndugu Libosso,

Chei chei. Salamu zangu za dhati zikufikie popote ulipo. Aisee, upo? Kwa heshima na tahadhima nachukua nafasi hii adimu, hati na kalamu, huku nikipunga hewa kuu mwanana wa bahari Hindi, kukuandikia waraka huu wa wasia.

Nimetumana sharubati ila ningependa pia kusema nawe kutoka mvungu wa moyo wangu! Nakuita na kusema nawe japo kwa utulivu na unyenyekevu: Ujana ni kama moshi na ukienda haurudi tena. La kwanza hilo.

Nikikusuta, basi hakikisha ujana wako umeishi maisha timilifu. Usiwe mwenye kasi wa kuiga wengine wanaoiga mengi ya nje, bali uwe mwenye kasi wa kuigwa—mfano wa kutajika kwa jamii. Miaka hii kila wakati ukumbuke kuwa cha msingi ni masomo, na kupata msingi wa maisha. Masomo yasiwe tu ya chaki na vitabu vyenye Kiingereza ngumu, kumbuka kila hatua kwa maisha ni funzo.

Kuwa makini. Kuna wengi walaghai. Humu, mnavyoita, *Facebook*, *Insta*na *Whatsapp* si pa kumuamini sana mtu. Usibabaike na kina kaka wanaopiga picha mbele ya magari za kifahari. Usibabaishwe na msichana aliyepiga picha huku kashika Biblia ukajua ndiye anaijua dini. Aisee, humu kwenye mitandao ya kijamii panatisha ndugu. Kuwa makini.

La pili. Jiamini maishani, kwani wewe ni bingwa. Kuna wengi wenye kisomo cha juu, ila akili zao zipo gerezani. Hawajaamini maarifa waliyonayo kuwa ndo muhimu kuliko vyeti walivyo navyo. Akili zako ziwe huru! Kwa maana hiyo, nakuomba kitu moja kaka: tumia vyeti vinapo hitajika, lakini pia viweke pembeni unapohitaji kutumia akili au nguvu.

Ila usisahau, siri ya mafanikio ni uvumilivu na kujituma katika kazi uifanyao. Uvune ya kheri wala sio ya shari.

Kaka, chini ya mnazi huu namwona mhudumu anawasili na sharubati baridi la maembe. Lakini nitakuwa sijakamilisha waraka huu nisipokukumbusha haya: Usidharau Mola wako, wazazi, wala waliokuzidi kwa umri.

Miaka hii utawapata mabinti kadhaa katika pilka pilka za maisha. Ukimpata binti wa kweli ambaye atakuwa kama mama kwako, mama kwa wanao na mama mlezi kwa familia, tafadhali kaka usimuache huyo! Mdhamini kwa moyo wako wote. Kukiwa na jambo, basi jaribuni kutatua changamoto zenu kwenye chumba chenu wenyewe, mbali na wanao na bila kila mara kwenda kwa watu au mitandao ya kijamii kuomba usuluhishi.

Nakuomba, msaidie huyu binti wako kutimiza ndoto zake kulingana na uwezo wako kama ambavyo unahangaika kutimiza ndoto zako. Na mkijaliwa kufunga pingu za Maisha, Mola awape watoto, basi mjitahidi nanyi muwape elimu na maadili njema.

Nafikia kikomo. Japo ninayo mengi ya kusema kutoka moyoni. Nalikunja jamvi langu. Waraka nautia kikomo. Nakuaga nikitumai wasia wangu utautilia maanani. Na ukiudharau, basi kesho utanililia.

Niweke mahali pema moyoni,

Kaka wa Baadaye - Libosso

Previous Next